NABII NI NANI KI-BIBLIA?

 JINSI YA KUWATAMBUA MANABII WA KWELI.

Katika somo hili nitaelezea jinsi ya kuwatambua manabii wa kweli wa Mungu kutokana na sifa walizokuwa nazo wakati wa Agano la Kale na Agano Jipya. Ni muhimu kila mkristo aliyeokoka aweze kupambanua (kutofautisha) na kutambua manabii wa kweli na manabii wa uongo. Manabii wa kweli walikuwa na sifa zifuatazo;


1.Walikuwa waaminifu. Hapa tutaangalia manabii watatu ambao ni Yesu, Musa na Samweli ambao walikuwa waaminifu katika mambo yote ya Mungu. Waebrania 3:1-2

“...Yesu aliyekuwa mwaminifu kwake yeye aliyemweka, kama naye Musa alivyokuwa, katika nyumba yote ya Mungu.” Katika andiko hili, Yesu amefananishwa na nabii Musa alivyokuwa mwaminifu. Mwingine ni Samweli, alipokuwa mzee aliwashuhudia wana wa Israel jinsi alivyokuwa mwaminifu tangu akiwa kijana. 1Samweli 12:2-4 “Basi sasa, angalieni, mfalme anakwenda mbele yenu; na mimi ni mzee, mwenye mvi; tena, tazameni, wana wangu wapo pamoja nanyi; nami nimekwenda mbele yenu toka ujana wangu hata leo.

Nami nipo hapa; basi, mnishuhudie mbele za BWANA, na mbele ya masihi

wake, nalitwaa ng’ombe wa nani? Au nalitwaa punda wa nani? Au ni nani niliyemdhulumu? Ni nani niliyemwonea? Au kwa mkono wa nani nimepokea rushwa inipofushe macho? Nami nitawarudishia ninyi.

Nao wakasema, hukutudhulumu, wala hukutuonea, wala hukupokea kitu kwa mkono wa mtu awaye yote.”


2.Walikuwa wakisema kile ambacho Mungu aliwaambia au kuwaonyesha bila kuongeza au kupunguza. 2Petro 1:

21 “Maana unabii haukutolewa popote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu”.


3.Walikuwa na bidii kuutafuta uso wa Mungu. Hapa nitawataja baadhi ya manabii ambao walikuwa wanaomba mbele za Mungu kwa bidii ambao ni; Yesu Kristo Bwana wetu, Eliya Mtishibi na Ana. Soma katika Biblia: Luka 22:41, Luka 2:36-37 na Yakobo 5:17-18.


4.Walikuwa wanyenyekevu na wenye hofu ya Mungu.


5.Walikuwa na huruma kwa ajili ya Taifa lao na kuliombea ili Mungu asilihukumu kutokana na makosa ambayo lilifanya. Hapa nitawataja baadhi yao ambao ni Musa na Samweli. Samweli 12:23

“Walakini mimi, hasha! Nisimtende BWANA dhambi kwa kuacha kuwaombea ninyi; lakini nitawaelimisha katika njia iliyo njema, na kunyoka.”  

Kutoka 32:31-32

“Musa akarejea kwa BWANA akasema, Aa! Watu hawa wametenda dhambi kuu wamejifanyia miungu ya dhahabu. Walakini sasa, ikiwa utawasamehe dhambi yao – na kama sivyo, unifute, nakusihi, katika kitabu chako ulichoandika.”


6.Waliyoyatabiri yalitimia. Lakini kwa nyakati hizi za mwisho ni muhimu kwa kila mwamini kuwa makini na kufahamu ya kwamba siyo kila nabii asemaye unabii ukatimia na kutenda miujiza ni nabii wa kweli. Kumbukumbu 13:1-3 “Kukizuka katika yako nabii, au mwotaji wa ndoto, akikutolea ishara au ajabu, ikatukia hiyo ishara au hiyo ajabu aliyokuambia, akisema, Na tuifuate miungu mingine usiyoijua, tuitumikie hiyo; wewe usiyasikilize maneno ya nabii yule, au yule mwotaji wa ndoto…”


Kutokana na andiko hili hapa juu linaonyesha wazi ya kwamba tunaweza kuwatambua manabii wanaopotosha kwa mambo yale wanayotuambia au kutuelekeza kinyume na neno la Mungu. Na ikiwa hawana matunda mazuri hao ni manabii wa uongo. Ndio maana imeandikwa; Mathayo 7:15-20 “Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa - mwitu wakali. Mtawatambua kwa matunda yao. Je! watu huchukua zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti? Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri. Kila mti usiozaa tunda zuri hukatwa ukatupwa motoni.

Ndiposa kwa matunda yao mtawatambua.” Mfano wa mti mwema ni yule mtu anayeyafanya mapenzi ya Mungu (matakwa ya Mungu). Na mfano wa mti mwovu ni mtu asiyeyafanya mapenzi ya Mungu.


7.Unabii walioutoa ulilingana na neno la Mungu. Haukupigana na neno la Mungu mahali popote katika biblia. Mwamini anaweza kuutambua unabii kwa kutumia neno la Mungu. Lakini ni lazima kwanza ayafahamu maneno ya Mungu na kuyahifadhi moyoni.

Wakolosai 3:16

"Na neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote…” Mtu akiwa na maneno ya Mungu kwa wingi moyoni anaweza kuyapima mambo yote ya Kiroho.


Jinsi ya kuwatambua manabii wa uongo. Ni kwa njia zifuatazo;

1. Tunaweza kuwatambua au kuwapambanua kwa tabia zao ambazo haziendani na neno la Mungu na ziko dhahiri wala haziwezi kufichika. Tunaweza kuwatambua kwa kutumia neno la Mungu na tunda la Roho.  

Wagalatia 5:22-23

“Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.”


2. Kuwatambua kwa mafundisho yao ya kibinadamu. Mafundisho yao wameyatunga hayaendani na neno la Mungu. Wanafundisha na kuhubiri kwa kutafsiri mistari ya biblia kinyume neno la Mungu. Kwa sababu hiyo wanakuwa wamewapotosha waamini katika njia ya Mungu. Hutumia mafundisho ya uzushi na uongo na kuyachanganya na maandiko ya neno la Mungu kana kwamba ni neno la Mungu. Kwa sababu hiyo huwapotosha wasiolijua neno la Mungu kwa ukamilifu. Ikiwa mwamini yuko makini na anayafahamu maandiko kwa ukamilifu ni lazima atagundua ya kwamba mafundisho wanayofundisha na kuyahubiri yanapingana na neno la Mungu katika biblia. Ndio maana imeandikwa tusiamini kila roho (kila nafsi) tuzijaribu kwanza. 1Yohana 4:1

“Wapenzi msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani.”


Mwalimu wa neno la Mungu.

Ni muhimu kuwa makini anapotafsiri mistari ya neno la Mungu katika biblia, ni lazima ahakikishe inaendana na maandiko mengine katika biblia. asichokijua kwa usahihi asiwafundishe watu na kuwapotosha ili asije akahukumiwa. Imeandikwa; Ufunuo wa Yohana 22:18-19

“Namshuhudia kila mtu ayasikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mtu ye yote akiyaongeza, Mungu atamwongezea hayo mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki. Na mtu ye yote akiondoa lo lote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mungu atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima, na katika ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki.” Kumbukumbu 4:2

“...neno niwaamurulo wala msilipunguze, mpate kuzishika amri za Bwana, Mungu wenu, niwaamuruzo.” Katika maandiko haya, Mungu ameonya tusije tukaongezea katika maneno yake ambayo yamekwisha kuandikwa. Kwa sababu hiyo hatupaswi kuchanganya neno la Mungu na mafundisho yetu ya kibinadamu. Pia ameonya tusiondoe wala kupunguza maneno ambayo yamekwisha kuandikwa kwenye kitabu chake.


Jambo lingine limpasalo mtu kutambua ni kwamba maandiko yaliyomo katika biblia ni maneno ya unabii. Ufunuo wa Yohana 22:19 “Na mtu ye yote akiondoa lo lote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mungu atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima, na katika ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki.”

Maneno ya unabii ni yale ambayo Mungu alisema na manabii wake kwa njia ya sauti, maono na ndoto, yakaandikwa katika biblia.

Kwa sababu hiyo mtu anapofundisha neno la Mungu anakuwa anafundisha maneno ya unabii. Kwa kufanya hivyo si kwamba ametoa unabii.


Unabii Unavyotokea

Nabii anatoa unabii kwa yale ambayo Mungu amesema naye kwa njia ya sauti, maono na ndoto. Hesabu 12:6-8

“Kisha akawaambia,

Sikizeni basi maneno yangu;

Akiwapo nabii kati yenu,

Mimi, BWANA, nitajifunua kwake katika maono,

Nitasema naye katika ndoto.

Sivyo ilivyo kwa mtumishi wangu, Musa;

Yeye ni mwaminifu katika nyumba yangu yote;

Kwake nitanena mdomo kwa mdomo, Maana, waziwazi wala si kwa mafumbo; Na umbo la BWANA yeye ataliona. Mbona basi ninyi hamkuogopa Kumnenea mtumishi wangu, huyo Musa?”


Tahadhari Kuhusu Kutoa Unabii.

Ni muhimu kila mkristo aliyeokoka kuwa makini ili asije akahukumiwa kwa mambo haya yafuatayo;

1.Usitabiri uongo

2. Usipokee unabii wa uongo. Yeremia 14:14,16

“Ndipo BWANA akaniambia, Hao manabii wanatabiri uongo kwa jina langu mimi; mimi sikuwatuma, wala sikuwaamuru, wala sikusema nao; wanawapeni unabii wa maono ya uongo, na uaguzi, na neno la ubatili, na hadaa ya mioyo yao. Na watu hao, waliopewa unabii na wao, watatupwa nje katika njia kuu za Yerusalemu kwa sababu ya upanga na njaa; wala hawatakuwa na mtu wa kuwazika, wao na wake zao, na wana wao, na binti zao; maana nitamwaga uovu wao wenyewe juu yao.” Yeremia 23:31-32

“Tazama, mimi ni juu ya manabii, asema BWANA, wanaotumia ndimi zao na kusema, Yeye asema, Tazama, mimi ni juu ya hao wanaotabiri ndoto za uongo, asema BWANA, na kuzisema, na kuwakosesha watu wangu kwa uongo wao, na kwa majivuno yao ya upuzi, lakini mimi sikuwatuma, wala sikuwapa amri; wala hawatawafaidia watu hawa hata kidogo, asema BWANA.”


3. Kuwa makini usiseme mambo ambayo Mungu hakusema na wewe kwa njia ya sauti, maoni na ndoto. Utakayoyasema hakikisha au thibitisha ni Mungu kweli amesema. Mungu anataka useme neno lake kwa uaminifu. Yeremia 23:28,31-32

“Nabii aliye na ndoto, na aseme ndoto yake; na yeye aliye na neno langu, na aseme neno langu kwa uaminifu. Makapi ni kitu gani kuliko ngano? Asema BWANA. Tazama, mimi ni juu ya manabii, asema BWANA, wanaotumia ndimi zao na kusema, Yeye asema, Tazama, mimi ni juu ya hao wanaotabiri ndoto za uongo, asema BWANA, na kuzisema, na kuwakosesha watu wangu kwa uongo wao, na kwa majivuno yao ya upuzi, lakini mimi sikuwatuma, wala sikuwapa amri; wala hawatawafaidia watu hawa hata kidogo, asema BWANA.”

Comments

Popular posts from this blog

UCHAWI KIUHALISIA

NDOTO NA MAANA ZAKE

UHALISIA ROHONI